Top Stories

ISN Magazine | Bilingual Edition (ENG/SW)

ISN Magazine | Bilingual Edition (ENG/SW)
ISN Weekly Sports Magazine – Free Access

Simba SC Yanyanyua Taji Zanzibar, Yanga SC Yalala Dakika za Jioni.

Wachezaji wa Simba SC wakishangilia ubingwa wa Muungano Cup 2026 dhidi ya Yanga SC

Zanzibar imeshuhudia historia mpya jana baada ya Simba SC kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Muungano Cup 2026 kwa kuifunga Yanga SC goli 1-0. Mchezo huo uliokuwa na vuta nikuvute ya mbinu, uliamuliwa na utulivu wa mchezaji mmoja tu aliyeweza kuitumia nafasi adimu iliyopatikana mwishoni mwa mchezo.

Shujaa wa usiku huo alikuwa Seleman Mwalimu, ambaye alizima kelele za mashabiki wa Yanga kwa mkwaju wa penati uliokwenda moja kwa moja nyavuni. Goli hilo la dakika za jioni lilikuja wakati kila mmoja akiamini kuwa mechi ingekwenda kwenye matuta, hali iliyoamsha shangwe nzito kwa mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi waliofurika uwanjani.

Ufundi wa Simba SC jana ulionekana zaidi kwenye eneo lao la ulinzi, ambapo walifanikiwa kuwazuia washambuliaji wa Yanga SC wasipate nafasi ya wazi ya kufunga. Licha ya Yanga kumiliki mpira kwa muda mrefu katikati ya uwanja, ukuta wa Simba ulibaki kuwa imara na kusubiri makosa ya wapinzani wao ili kufanya mashambulizi ya kushtukiza.

Ushindi huu siyo tu taji la Muungano, bali ni ujumbe mzito kwa wapinzani wao kuwa Simba SC bado ni tishio kwenye michuano mikubwa nchini. Picha za wachezaji wakishangilia na kombe hilo zinaonyesha kurejea kwa morali na hali ya kujiamini ndani ya kikosi hicho kuelekea kumalizika kwa msimu wa ligi.

Tathmini ya ushindi huu ni hatua muhimu kwa Simba SC katika kujiimarisha kisaikolojia kuelekea mechi ya ligi kuu Tanzania bara itakayo wakutanisha tena miamba hiyo ya soka baada ya presha kubwa ya mashabiki ya kipindi kirefu. Kwa upande wa Yanga SC, kupoteza taji hili dakika za mwisho ni darasa tosha kuwa umakini unahitajika kuanzia filimbi ya kwanza mpaka ile ya mwisho.

Comments